11 Novemba 2023 - 17:45
Ansarullah ya Yemen yakosoa vikali ulegevu walioonyesha watawala wa Kiarabu mbele ya Wazayuni

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imesisitiza kuwa itaendelea kuliunga mkono kwa dhati taifa na Muqawama wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na imekosoa vikali udhaifu na ulegevu ulioonyeshwa na watawala wa nchi za Kiarabu mbele ya utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel.

Shirika la habari la Tasnim limeripoti leo kuwa Muhammad Abdusalam, msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema: jukumu dogo kabisa ambalo mfumo wa Kiarabu na Kiislamu unapaswa kutekeleza ni kuchukua hatua kwa namna itakayoweka kizuizi cha kuwazuia Wazayuni wasifanye jinai zao. 

Abdusalam ameeleza bayana kuwa: "lau kama Wazayuni wangeona watawala wa Kiarabu wamechukua msimamo imara dhidi yao, wasingethubutu kufanya jinai hizi".

Msemaji wa Ansarullah ya Yemen amebainisha kuwa, wao kwa upande wao huko Yemen wanatimiza wajibu wao kwa Mwenyezi Mungu na kwa Palestina kwa gharama na thamani yoyote ile.

Aidha, Muhammad Abdusalam amesema, ana matumaini kuwa Waarabu na Waislamu wataangalia upya na kwa kina misimamo yao na kuelewa kwamba ulimwengu huu unamheshimu mtu anayejiheshimu yeye mwenyewe tu, taifa lake na suala lake linalomhusu.../

.342/